MAMLAKA YAWEKEZA BILIONI 38 KWENYE MITAMBO NA VIFAA VYA MAABARA

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema kwa kipindi cha miaka mitano Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewekeza takribani Shilingi Bilioni 38 kwenye ununuzi wa mitambo ya kisasa ya uchunguzi na vifaa vya maabara.
Dkt. Mafumiko ameyasema hayo Oktoba 8, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha utekelezaji na tathmini ya watoa huduma za mitambo na vifaa vya Maabara kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
“Katika kutekeleza jukumu hili la uchunguzi wa kimaabara, Mamlaka imeendelea kuboresha miundombinu ya Maabara kwa kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kisasa, vipuri na matengenezo. Mfano katika kipindi cha miaka mitano Mamlaka imetumia takribani billion 38 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya maabara.
Fedha hizo ni nyingi kiasi cha kutukumbusha kuweka mikakati sahihi ya namna bora ya kuilinda mitambo hiyo. Mtambo unaoendeshwa kwa usahihi na kutunzwa vizuri unakuwa na uhakika wa kutumika kwa muda mrefu na hivyo kuokoa fedha nyingi za taasisi. Pamoja na gharama kubwa za uendeshaji, tunalazimika kwenda na kasi ya teknolojia iliyopo sasa. Mbinu pekee inayoweza kutunusuru ni kujenga uwezo mkubwa wa kutunza mitambo yetu tunayomiliki” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali, amewataka wataalam kutoka Kitengo cha Huduma za Ufundi kujengeana uwezo na wataalam wengine katika matumizi ya mitambo kulingana na uzoefu na ujuzi wa matumizi ya mitambo hiyo kwa muda mrefu.
“Ni dhahiri kwamba mtu hawezi kuwa mahiri katika mambo yote kwa wakati wote. Unaweza ukawa mahiri sana kutumia mtambo wa LC-MS/MS na usiwe bora kwa kiwango hicho katika kufanya uchunguzi kwa kutumia mtambo wa GC/MS/MS. Kwa kuwa nyinyi watumishi wa Kitengo cha Huduma za Ufundi tumewapa jukumu la kusimamia mitambo, tunategemea muwe na utaratibu wa watu kujengeana uwezo, ili kila mmoja awe na ufahamu wa kiwango kizuri katika kusimamia mitambo na vifaa vilivyopo maabara” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma za ufundi, Francis Kway, alisema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili changamoto za watoa huduma za matengenezo kinga, vipuri na kubadilika mara kwa mara kwa watoa huduma za mitambo. Hivyo, wanapaswa kujadili na kuja na mapendekezo ya utekelezaji ili kuboresha huduma za mitambo ya uchunguzi wa kimaabara.