Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA YANG’ARA RIADHA NA MBIO ZA MAGUNIA SHIMMUTA

Imewekwa: 26 Nov, 2023
MAMLAKA YANG’ARA RIADHA NA MBIO ZA MAGUNIA SHIMMUTA

Wanamichezo wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), wameng’ara katika Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (Shimmuta 2023), yaliyofanyika kuanzia Novemba 12 hadi 26, 2023 jijini Dodoma, baada ya kufanya vizuri katika mbio za magunia na riadha.

Katika mashindano hayo, Mamlaka imeibuka mshindi wa pili kwenye mchezo wa mbio za gunia, mshindi wa pili kwenye riadha (wanawake) mita 800 na mshindi wa tatu kwenye riadha (wanawake) mita 5000.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Makamu Mwenyekiti wa Michezo GCLA, Sabas Mandari amesema kuwa ushindi huo ni uthibitisho kuwa uongozi wa Mamlaka unathamini michezo, hivyo kuwezesha watumishi kushiriki mashindano ya Shimmuta. Pia, amempongeza Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko kwa ushirikiano wake katika kuhakikisha michezo inapewa kipaumbele.

“Nichukue nafasi hii kumshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye amekuwa nasi bega kwa bega kuanzia wakati wa maandalizi, wakati wa safari na kutupokea Dodoma pamoja na kutupa hamasa,” alisema Mandari.

Aidha, Makamu Mwenyekiti amemshukuru Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Evaclotida Kapinga kwa mchango wake kwa wanamichezo wa Mamlaka ikiwa na yeye mwenyewe mwanamichezo ambaye alijitahidi kutupa hamasa ya kutupa moyo, pia alicheza  kwa kujituma licha ya kwamba ni kiongozi.

Aidha, amewapongeza wanamichezo kwa namna walivyojitoa muda wote wa mashindano mpaka mwisho na kuwasihi kutokata tamaa kwani anaamini mwakani wanamichezo wa Mamlaka watafanya mambo makubwa zaidi na kupaisha jina la taasisi.

Mandari, ametoa rai kwa watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukulia michezo kama ni ya kila mmoja kwani michezo ni urafiki, michezo ni afya na kupitia michezo kila mmoja anaweza kuboresha utendaji wake wa kazi.

Kadhalika, amewashukuru watumishi wa Mamlaka waliopo Dodoma kwa kuonesha upendo kama familia moja ya GCLA kwa kufika kwenye viwanja mbalimbali kushangilia timu za Mamlaka zilipokuwa zikicheza.

Katika mashindano hayo, timu ya mpira wa pete ya Mamlaka kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kuingia katika hatua ya 16 bora.