Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MAONESHO YA MADINI GEITA

Imewekwa: 09 Oct, 2023
MAMLAKA YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA MAONESHO YA MADINI GEITA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeibuka mshindi wa kwanza kwenye maonesho ya Sita ya Madini mkoani Geita katika kipengele cha Taasisi Wezeshi za Serikali katika Sekta ya Madini.

Tuzo hizo zilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika siku ya kilele cha maonesho hayo yaliyohitimishwa Septemba 30, 2023 katika viwanja vya EPZA, Bombambili mkoani Geita.

Akiongea baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Sabanitho Mtega, amewapongeza watumishi wote walioshiriki maonesho hayo kwa moyo wao wa kujituma kuhudumia wadau na wananchi mbalimbali waliotembelea banda la Mamlaka bila kuchoka na kutoa huduma nzuri iliyopelekea kuibuka washindi katika kipengele husika.

“Nawapongeza kwa ushindi huu ambao tumeupata kutokana na kazi kubwa tuliyofanya katika siku kumi za kuhudumia wananchi na wadau wa Geita na maeneo ya Jirani katika maonesho haya ya madini. Haikuwa kazi ndogo kuhudumia watu zaidi ya elfu mbili mia tano kwa siku hizi, tena kwa moyo mkunjufu na huduma bora kwa mteja ambayo naamini ndio iliyowawezesha majaji kuona tunastahili kuwa washindi katika kipingele hiki. Naamini ushindi huu ni chachu kwa maonesho mengine tutakayoshiriki siku zijazo kwa maana ya kuzingatia mazuri yote yaliyotuwezesha kushinda katika maonesho haya na kuboresha zaidi ili kuendelea kuwa katika Nafasi hii” alisema.

Naye Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa, Musa Kuzumila, alitoa shukrani kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuridhia Mamlaka kushiriki maonesho hayo kama sehemu ya wadau wakubwa wa sekta ya madini, hivyo maonesho hayo yamesaidia pia kukutana na wadau na kuwapatia elimu kuhusu matumizi salama ya kemikali na kusaidia kusajili wadau ambao wanajishughulisha na matumizi ya kemikali ambao bado hawajasajiliwa na kusajili wadau wapya ambao wanahitaji kuingia kwenye biashara ya kemikali na uchimbaji wa madini. Hivyo, mbali ya ushindi huo wa tuzo,pia inasaidia Mamlaka kujitangaza na kusaidia wadau wake ambao wanatembelea kwenye maonesho.