Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA IMEPIGA HATUA KATIKA UKAGUZI WA KEMIKALI NCHINI

Imewekwa: 14 Jun, 2024
MAMLAKA IMEPIGA HATUA KATIKA UKAGUZI WA KEMIKALI NCHINI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imefanya Mkutano Mkuu wa Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia kwa lengo la kuwapa nafasi wakaguzi kujadili kwa kina masuala mbalimbali muhimu yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za viwandani na majumbani.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mamlaka jijini Dodoma Juni 9, 2024, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amewataka wakaguzi wa kemikali kuzingatia wajibu wao katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za viwandani na majumbani Sura 182 pamoja na Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya mwaka 2016.

“Mkutano huu unatarajiwa kutathmini utendaji wetu pale tulipo, naomba mtambue kuwa ninyi ni nyenzo muhimu sana katika kutekeleza sheria ya kemikali pamoja na kanuni zake. Wengi wenu mnafanya vizuri sana katika usimamizi na utekelezaji wa sheria hii,” alisema Dkt. Mafumiko.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo amewasihi wakaguzi kuendela kufanya kazi kwa kujituma na kutanguliza uzalendo katika suala zima la ukaguzi wa wadau wa kemikali hivyo kuongeza juhudi na ufanisi kwenye kutekeleza majukumu yao ya ukaguzi ili kuendelea kulinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Kwa upande wake Mkaguzi kutoka Mamlaka, Msafiri Mwasyeba alipendekeza kuwa Mamlaka kushirikisha wadau kutenga maeneo mahususi ya kupaki magari yanayobeba kemikali hatarishi ili kuweza kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza kama kutokea kwa mlipuko ambao ni hatari kwa usalama wa nchi.

Pia, Mkaguzi mpya wa kemikali kutoka Ofisi ya Kanda ya Mashariki, George Petro amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko kwa kuwaamini na kuahidi kuendelea kujituma usiku na mchana ili kufikia malengo ya Mamlaka.

“Sisi kama watumishi wapya tutatumia nguvu zetu na akili ili kutimiza majukumu tutakayopangiwa. Tunashukuru kwa kushiriki katika mkutano huu ambao tumeweza kukutana na watumishi wenzetu kutoka kanda mbalimbali, sisi tutaitumia kama motisha ya kujifunza zaidi na kutusaidia katika utendaji kazi,” alisema Petro.