MAFUNZO YA WACHUNGUZI WA VINASABA YAIMARISHA UZINGATIAJI WA SHERIA, UBORA NA USIRI WA TAARIFA
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendesha mafunzo ya siku tatu kwa Wachunguzi wa Maabara za Sayansi Jinai na Vinasaba vya Binadamu kwa lengo la kuimarisha uelewa, weledi na uwezo wao katika kufanya uchunguzi kwa kuzingatia sheria, viwango vya kitaalamu, udhibiti wa ubora na usalama wa taarifa za vinasaba vya binadamu.
Mafunzo hayo yaliyofanyika ukumbi wa Mkemia, jijini Dar es Salaam, kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2026, yaliwakutanisha wachunguzi kutoka Jeshi la Polisi wanaohusika na uchunguzi wa sayansi jinai na vinasaba vya binadamu, huku yakilenga kuongeza ujuzi katika utekelezaji wa majukumu ya kiuchunguzi pamoja na kuimarisha uzingatiaji wa matakwa ya kisheria.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, aliwataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya kisheria, kitaalamu na kiuchunguzi yanayohusiana na Vinasaba vya Binadamu.
“Uchunguzi wa Vinasaba vya Binadamu unapaswa kufanyika kwa kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni, miongozo na viwango vya kitaalamu vilivyowekwa. Weledi wa mchunguzi unahitajika katika kila hatua ya mchakato wa uchunguzi, kuanzia ukusanyaji, upokeaji na utunzaji wa sampuli, uchambuzi na tafsiri ya matokeo hadi utoaji wa taarifa, huku taratibu za usiri na usalama wa taarifa zikizingatiwa wakati wote” alisema Elias.
Elias alisema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni Msimamizi na Mtekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Vinasaba vya Binadamu Na. 8 ya mwaka 2009 (Sura ya 173), pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019, zinazoweka msingi wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli zinazohusiana na vinasaba vya binadamu. Alisisitiza kuwa uelewa wa matakwa hayo ya kisheria ni muhimu kwa kila mchunguzi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa usahihi, huku akizingatia wajibu na mipaka ya kitaalamu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Baiolojia na Vinasaba kutoka Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Polisi Makao Makuu, Lutengano Mwanginde, alisema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa kwa washiriki kutokana na fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu katika eneo la vinasaba vya binadamu.
“Tumeyafurahia sana mafunzo haya kwa sababu tumepata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu mahiri na wenye uzoefu. Tunatarajia kutumia maarifa na ujuzi tunaoupata kuongeza tija na kuimarisha utendaji wa Maabara ya Vinasaba ya Jeshi la Polisi Tanzania,” alisema Mwanginde.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wanaohusika na uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na matakwa ya sheria, viwango vya kitaalamu na misingi ya usiri, usalama na uadilifu wa taarifa za vinasaba.