Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAAFISA WA POLISI WAPEWA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA SAMPULI ZA JINAI

Imewekwa: 16 Mar, 2026
MAAFISA WA POLISI WAPEWA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA SAMPULI ZA JINAI

Wataalamu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) wametoa mafunzo kwa askari wa Jeshi la Polisi kuhusu usimamizi wa sampuli za makosa ya jinai, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha matumizi ya sayansi katika upelelezi na utoaji wa ushahidi mahakamani.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam Machi 12, 2026, yamelenga kuwajengea uwezo askari katika ukusanyaji, utunzaji na usafirishaji sahihi wa sampuli za jinai kutoka eneo la tukio hadi maabara kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Dkt. Lazaro Mambosasa, alisema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni muhimu katika kuhakikisha ushahidi wa kisayansi unatumika ipasavyo katika upelelezi wa makosa ya jinai.

“Moja ya majukumu makubwa ya Jeshi la Polisi ni kufanya upelelezi wa makosa ya jinai. Katika mchakato huo tunashirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambayo ina jukumu muhimu la kuchambua sampuli na kutoa majibu ya kisayansi yanayotumika kama ushahidi mahakamani,” alisema Dkt. Mambosasa.

Alifafanua kuwa sampuli zinazokusanywa kutoka katika maeneo ya matukio ya uhalifu ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazotumika kuthibitisha makosa ya jinai mahakamani, kwani husaidia kumuunganisha mtuhumiwa na tukio lililotendeka kupitia ushahidi wa kisayansi.

“Unapozungumzia sampuli, unazungumzia moja ya nyenzo muhimu za ushahidi. Hizi ndizo zinazosaidia kuthibitisha kosa mahakamani ili pale ambapo mtuhumiwa anapatikana na hatia, ahukumiwe kwa mujibu wa sheria,” alieleza.

Dkt. Mambosasa alisisitiza kuwa uchunguzi wa kisayansi una nafasi kubwa katika mfumo wa kisasa wa upelelezi wa makosa ya jinai, akibainisha kwamba kesi isiyofanyiwa uchunguzi wa kisayansi ipasavyo inaweza kuondolewa mahakamani kwa kukosa ushahidi wa kumuunganisha mtuhumiwa na kosa linalodaiwa kutendeka. Ndiyo maana mafunzo haya yanayotolewa na wataalamu wa GCLA ni muhimu sana kwa askari wa jeshi la Polisi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Isaya Mayagila aliwashukuru wataalamu wa GCLA kwa kuwapatia mafunzo yaliyowaongezea uelewa kuhusu usimamizi wa sampuli za ushahidi katika uchunguzi wa makosa ya jinai.

“Mafunzo haya yametupatia maarifa muhimu kuhusu namna sahihi ya kukusanya, kuhifadhi na kusafirisha sampuli za ushahidi. Tutaenda kuyatumia kikamilifu katika maeneo yetu ya kazi ili kuongeza ufanisi wa upelelezi,” alisema.

Wakati huo huo, wananchi wametakiwa kushirikiana na vyombo vya dola kuepuka kuingilia eneo la tukio la uhalifu, hatua ambayo inaweza kusababisha kupotea au kuvurugika kwa ushahidi muhimu.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Jeshi la Polisi katika matumizi ya sayansi ya uchunguzi wa jinai ili kusaidia upatikanaji wa ushahidi na kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.