KANDA YA KATI YAIMARISHA USIMAMIZI WA MAABARA ZA KEMIA
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, amewataka wadau wa kemikali wa Kanda ya Kati kufanya usajili wa Maabara za Kemia ili kuepusha uchepushaji wa kemikali katika utengenezaji wa dawa.
Mkurugenzi Ndiyo amesema hayo Machi 31,2026, jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya Udhibiti na Usimamizi wa Maabara za Kemia kwa wadau wa kemikali kutoka Kanda ya Kati yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kati.
“Kitu cha kwanza ambacho naweza kuzungumzia kwenu wadau inabidi tujitahidi sana kuzifanya kazi zetu kuwa rasmi kwa kufanya usajili wa hizi maabara na bidhaa zetu za kemikali, kwa sababu uhifadhi wa kemikali unahitaji umakini wa hali ya juu na pia wataalamu ambao watakusaidia kukupatia maelekezo ya namna gani unatakiwa kuhifadhi kemikali kwa uangalifu, Pia, itasaidia kupunguza uwepo wa kemikali hatarishi kwa jamii” alisema Daniel Ndiyo.
Naye Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga, amewashukuru wadau kwa kuweza kuhudhuria mafunzo hayo ambayo moja kwa moja yameweza kuzungumzia Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali na usimamizi wa Maabara za Kemia, huku akisema kuwa mafunzo hayo yatawajenga katika kufanya kazi za uzalishaji na utumiaji wa kemikali kwa usahihi katika maabara zao.
“Tumeandaa mafunzo haya ili kuweza kukutana na wadau wa Maabara za Kemia kutoka Kanda ya Kati ili kuwawezesha kuwapa elimu ya Sheria ya Usimamizi na udhibiti wa Kemikali pia inahusika na usimamizi wa maabara za kemia. Kwa kifupi imetupatia fursa ya kuwapa elimu namna gani wanaweza kusajili kemikali zao na namna wanatakiwa kufuata sheria ya kemikali na pia tumeweza kuchukua maoni yao kuhusu sheria ya kemikali na tutaenda kuyafanyia kazi” alisema Magdalena.