KAMISHNA JENERALI AIPONGEZA GCLA KWA KUTOA MATOKEO YA UCHUNGUZI KWA WAKATI

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiboresha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hali iliyochochea utolewaji wa majibu ya uchunguzi wa kimaabara kwa wakati.
Kamishna Jenerali Lyimo, amesema hayo Julai 5, 2025 wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam “Sabasaba” yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Tunaishukuru Serikali ya `awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiboresha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vya kisasa ambapo sasa hivi unapopeleka sampuli mbalimbali unapata majibu kwa wakati jambo linalorahisisha kupeleka mashtaka mahakamani kwa haraka na kusaidia haki kuweza kupatikana” alisema Lyimo.
Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwani ndiye mdau mkubwa wa kuweza kukamilisha majalada ya Mamlaka hiyo.
“Tunamshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutupa ushirikiano mkubwa kwani ndiye mdau mkubwa wa kuweza kukamilisha majalada ya Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya kwasababu ilikesi iweze kukamilika ni lazima tupate cheti kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, na tunashirikianae katika oparesheni mbalimbali za kupambana na kudhibiti dawa za kulevya” alisema Lyimo.
Naye Mkurugenzi wa uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt Peter Shimo, ameishukuru Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ushirikiano mkubwa inaotoa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kukamilisha mnyororo wa haki Jinai katika upatikanaji wa haki kwa wakati.
“Tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka DCEA kwani ni jukumu letu sote katika mnyororo ule wa haki Jinai, tunaendelea kuwekeza katika mitambo na kuboresha mbinu za uchunguzi na tunaishukuru Serikali kwa kutuongezea watumishi na kuwekeza katika Taaluma zao ili kuongeza ufanisi katika utendaji” alisema Dkt. Shimo