Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

HAKUNA SABABU YA KUSHINDWA KUWASAIDIA WANANCHI KWA KUKOSA UELEWA WA TARATIBU

Imewekwa: 05 Mar, 2024
HAKUNA SABABU YA KUSHINDWA KUWASAIDIA WANANCHI KWA KUKOSA UELEWA WA TARATIBU

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Fatma Nyangasa, amesema kuwa Serikali inatumia fedha, muda na raslimali watu kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaelimika na kupata uelewa wa  pamoja juu ya shughuli inazozitekeleza.

Mhe. Nyangasa ameyasema hayo Machi 4, 2024 wakati akifungua mafunzo ya Utekelezaji wa Sheria za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe  Mkoa wa Pwani.

“Mafunzo haya ya Utekelezaji wa sheria za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali yametusaidia sana kwani kabla ya hapo hatukuwa na uelewa mzuri juu ya kazi zinazofanywa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.   Sisi tunapata kesi nyingi za Watoto waliobakwa na nyinginezo, hivyo kupitia mafunzo haya tumeona hakuna sababu ya kushindwa kumsaidia mwananchi wa kawaida kwa kutokujua taratibu” alisema.

 Hata hivyo, Mhe. Mkuu wa Wilaya amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kuwezesha Mamlaka kununua mitambo ya kisasa ya gharama kubwa na hivyo kurahisisha utendaji kazi na upatikanaji wa haki kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Ubora wa Bidhaa na Mazingira, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega, amesema kuwa Mamlaka imekuwa ikitoa mafunzo kwa wadau na watumishi wa Serikali ambao wanashirikiana nao katika shughuli mbalimbali.

“Ni vibaya sana kudhani kila mmoja anajua majukumu unayofanya, lakini kwa mafunzo haya yatasaidia kujua Mamlaka inafanya nini na huduma gani zinatolewa, na wapi wanakoweza kuzipataalisema Mtega.

Mbali na mafunzo hayo  Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, pia imetoa vitakasa mikono (Sanitizer) na kuvikabidhi kwa uongozi wa Halmashauri hiyo ili vitumike katika kuwasaidia kujikinga na maambukizi mbalimbali.