Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAZIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU WA KEMIKALI

Imewekwa: 06 Dec, 2025
GCLA YAZIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU WA KEMIKALI

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kisirye Ukio, ametoa rai kwa wadau wa kemikali kuzingatia Sheria na Miongozo zinazosimamia masuala ya kemikali ili kuepuka madhara  kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwani madhara huweza kutokea endapo sheria zisipozingatiwa.

Mganga Mkuu ametoa rai hiyo wakati akifunga mafunzo ya mwaka ya uimarishaji kwa wasimamizi wa kemikali yaliyofanyika kwa siku 3 kuanzia Desemba 1 hadi 3, 2025 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani.

“Ni jukumu lenu kuhakikisha mnakuwa mstari wa mbele kulinda afya zenu, za wengine pamoja na mazingira na ili haya yote yatimie, mnatakiwa kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya matumizi yaliyo sahihi na salama ya kemikali,” alisema Ukio.

Pia, ameisihi Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iendelee kutoa elimu ya madhara ya kemikali kwa kuwafikia wadau mbalimbali wa kemikali pamoja na wananchi wa kawaida.

Kwa upande wake Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kutoka kwenye kampuni binafsi, taasisi za Serikali na kuwataka waendelee kutoa ushirikiano kwa Mamlaka jambo ambalo litasaidia katika kutekeleza Sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Pia, Mkapa ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo Mamlaka imepata mafanikio makubwa ya kuwa karibu na wadau wa kemikali.

Sambamba na hayo, Meneja Mkapa amesema kuwa matarajio ya taasisi ni kwamba mafunzo waliopata wataenda kufanyia kazi na kupitia hayo shughuli za Mamlaka zitaimarika katika nyanja zote ambazo wanahusika kwa namna moja au nyingine.

Naye mdau wa kemikali, Naomi Sonyo, ameipongeza Mamlaka kwa kuendeleza semina za kila mwisho wa mwaka kwa sababu inawakumbusha na kuwajengea mbinu mpya za kukabiliana na kemikali hatarishi.