GCLA YAWAITA WAKULIMA KUFAHAMU UBORA WA MAZAO

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewataka wadau mbalimbali wanaojishughulisha na kilimo kutembelea banda la Mamlaka ili waweze kupata elimu ya ubora wa mazao kabla ya kuingia sokoni kwa kuzingatia afya za walaji lakini pia na kujiimarisha kiuchumi.
Hayo yamesemwa Agosti 8, 2025 na Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati, Dodoma, Magdalena Mtenga, katika Maonesho ya Wakulima Nanenane ambayo kitaifa yamefanyika katika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma.
“Nichukue fursa hii kuwaita wadau mbalimbali wanaojishughulisha na kilimo kutembelea banda la Mamlaka kujifunza majukumu na kazi mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka hii ambayo imepewa dhamana na Serikali ya kuwahudumia wananchi kupitia masuala ya kijamii, Afya pia na masuala ya jinai kwa kuwa tunashughulika pia na uchunguzi wa jinai.
Pia, waje tuweze kuwapatia elimu ambayo itawasaidia kufahamu ubora wa mazao kwa namna gani yanatakiwa yawe na ubora wa kitaifa na kimataifa kabla ya kuyapeleka sokoni, hii itasawasaidia pia kujiimarisha kiuchumi lakini na kuhakikisha Afya na usalama wa walaji uko salama”. alisema Meneja Mtenga.
Akizungumzia lengo la Mamlaka kushiriki maonesho hayo, Meneja Mtenga amesema ni kujumuika pamoja na wadau na wananchi kwa ujumla kuwapa elimu kuhusu majukumu mbalimbali yanayofanyika katika Mamlaka ili yaweze kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku, lakini pia kwa kuwa Mamlaka imepewa jukumu la kutoa elimu kwa wadau, wananchi na jamii, kuangalia ubora wa mazao na bidhaa mbalimbali za viwandani na majumbani lakini pia hata kwa wafanyabiashara kuwa na uhakika wa ubora wa bidhaa zao zinazoingia sokoni.
Kwa upande wake Patric Maliyabwana ambaye ni Mkurugenzi kutoka kampuni ya Patric Decoration, ameipongeza Mamlaka kwa jitihada za kuhakikisha inawafikia wadau wengi na kuwapatia elimu kuhusu majukumu inayotekeleza, pia amewashauri wadau mbalimbali kutembelea banda la Mamlaka na Ofisi zake ili waweze kupata maelezo na kujifunza zaidi.
“Nina furaha kubwa na nina shukuru sana kwa maswali ambayo nimeuliza hapa na jinsi nilivyojibiwa, nikiri kwamba kuna vitu nilikuwa sivifahamu lakini kupitia maonesho haya ya Nanenane nimefahamu majukumu makubwa ya taasisi hii ikiwemo masuala ya uhalali wa mtoto kwa mzazi. Niwashauri wadau mbalimbali waje kwenye banda hili watajifunza na kufahamu mambo mengi sio tu kwenye kilimo lakini hata katika maswala ya Afya na ujasiliamali,” alisema Maliyabwana.