GCLA YATOA HUDUMA KATIKA MAONESHO YA MADINI GEITA

Mamlaka ya Maaabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema imejipanga kikamilifu kutoa huduma bora kwa wadau na wananchi mbalimbali wanaofika katika Banda la Mamlaka katika Monesho ya Kitaifa ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.
Hayo yamesemwa Septemba 21, 2025 na Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Maabara za Sayansi jinai na Vinasaba vya Binadamu, Fidelis Segumba katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.
“Sisi kama Mamlaka ya Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tuna wajibu wa kuwaelimisha wahusika wote ambao wanahusika na matumizi ya kemikali, na shughuli hizi za uchimbaji wa madini zinahusika kwa kiasi kikubwa sana na matumizi ya kemikali.
Kwa hiyo sisi kama wasimamizi wakuu kupitia sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za Viwandani na Majumbani tunalo jukumu la kuweza kutoa elimu kwa wadau hawa kuhusu matumizi sahihi na salama ya kemukali, lakini pia tutawapa elimu bora kuhusu majukumu mengine yanayotekelezwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali” alisema Segumba.
Kwa upande wake Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John wanjala amesema lengo la kushiriki maonesho hayo ni kuwasogezea karibu huduma wadau na wananchi lakini pia kukutana nao kwa karibu na kutatua changamoto zao.
“Tumekuwa tukishiriki maonesho ya Kitaifa ya Madini kila mwaka kwa sababu ya umuhimu wa shughuli tunazozifanya kama Mamlaka, hususan katika Usimamizi na kutoa elimu katika matumizi ya kemikali. Lakini pia tuko hapa kwa sababu wadau wengi waliopo hapa ni wadau wanaotumia kemikali kwa wingi lakini wengine wana changamoto ambazo pengine wanashindwa kuzifikisha tunapokuwa katika Ofisi zetu, kwa hiyo tukiwa hapa tunakuwa tumewasogezea huduma karibu ambayo wale wenye changamoto tuko hapa kuwasaidia” alisema Wanjala.