GCLA YASHINDA TUZO MBILI MAONESHO YA MADINI GEITA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeshinda tuzo mbili katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita.
Tuzo hizo zilizotolewa Septemba 27, 2025 ni pamoja na tuzo ya Mshindi wa pili kwa Taasisi za Umma katika Udhibiti, na Tuzo ya pili ni Tuzo ya Mshindi wa tatu kwa Taasisi Wezeshi za Serikali katika Sekta ya Madini.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Maabara za Sayansi jinai na Vinasaba vya Binadamu, Fidelis Segumba, amesema ushirikiano mzuri uliokuwepo kwa watumishi wote wa Mamlaka katika Maonesho hayo pamoja na kutoa elimu kwa jamii bila kujali makundi ndio ulifanikisha kupata ushindi huo.
“Kwa kweli inatupa furaha sana sisi kama watumishi ambao tumeiwakilisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hapa kwenye Maonesho haya Geita. Tumefurahi sana kwa sababu imeonesha ni kwa namna ambavyo kwa muda huu mfupi tumeweza, tumejituma katika kazi ya kuwaelewesha na kuwasikiliza wadau wote ambao walifanikiwa kufika na tukawapa huduma.
Kikubwa ninachoweza kusema ambacho kimejidhihirisha mpaka kupata ushindi huu wa tuzo mbili, ni namna ambavyo tumekuwa na ushirikiano mkubwa sana baina yetu sisi wenyewe katika kufanya kazi hii ya kuelewesha jamii bila kujali ni makundi ya aina gani kwa sababu tumetembelewa na makundi ya watu wa aina mbalimbali” alisema Segumba.
Kwa upande wake mtumishi wa Mamlaka kutoka Ofisi ya Kanda ya Ziwa Boaz Mizar, amesema jitihada katika kazi na kuwa karibu na wateja bila ya kubagua ndio nguzo ya mafanikio.
“Kwanza niwapongeze watumishi wote kwa jitihada walizofanya kukaribisha watu, kutoa elimu kwa Umma na kuelezea majukumu ya Mamlaka ili Umma ufahamu kwamba GCLA inafanya nini. Tumefanya kazi kwa ushirikiano baina yetu lakini pia kuwa na ukaribu na wadau wetu, naomba niseme tu kwamba unapofanya kazi jitihada zinaonekana, sasa baada ya majaji kupita zimeonekana jitihada zetu na matokeo ni kwamba tumeshinda tuzo hizi mbili” alisema Boaz.
Naye mtumishi wa Mamlaka kutoka Kanda ya Kati Dodoma, Abedinego Lugaila, amesema ari, nguvu na mwamko mkubwa wa watumishi wote katika Maonesho hayo katika kutoa elimu kwa Umma ndio silaha ya mafanikio.
Tuzo hizo zimekabidhiwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, ikiwa ni sehemu kubwa kwa mchango wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kutoa elimu ya udhibiti na Usimamizi wa kemikali kwa wadau wa madini.
Kupitia tuzo hizo Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha nafasi yake muhimu katika Uthibiti na Usimamizi wa Kemikali pamoja na kuwa mchango mkubwa wa sekta hiyo katika pato la Taifa.