GCLA YAPONGEZWA KWA KUWA CHACHU YA UPATIKANAJI WA WANASAYANSI TANZANIA

Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa tuzo kwa Wanafunzi na Walimu bora zaidi kitaifa wa masomo ya sayansi katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2023 na kidato cha sita mwaka 2024.
Dkt. Nyembea ameyasema hayo Juni 12, 2025 akimuwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, katika hafla ya kuwatunuku tuzo Wanafunzi na Walimu bora zaidi wa somo la Fizikia, Kemia, Baiolojia na Hisabati kidato cha nne 2023 na kidato cha sita 2024, iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Jubilee jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa tuzo hizo zina tija kubwa kwani ni chachu na zinadhihirisha kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi na kuhamasisha vijana kupenda masomo ya Sayansi.
“Tukio hili lina tija kubwa sana kutokana na uwepo wa majanga mbalimbali ya kidunia ambapo watalamu wa Sayansi wamekuwa na mchango mkubwa katika kuyapatia ufumbuzi, na katika Serikali ya awamu ya sita wataalamu hawa wanahitajika kwa wingi kwenye sekta ya Afya na suala la kupata wataalamu hawa halina mbadala” alisema Dkt. Nyembea.
Katika hatua nyingine Dkt. Nyembea amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mazingira wezeshi kwa kujenga Madarasa, Maabara na kuajiri Walimu ili wanafunzi wa masomo ya Sayansi waweze kufanya vema na Taifa letu liweze kupata wataalamu wa kutosha.
Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema lengo la tuzo hizo ni kujenga hamasa ya kupenda masomo ya Sayansi kwa kuwa yana mchango mkubwa sana katika Taaluma ya Afya ambayo wataalamu wake wanatokea katika masomo mama ya Sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia, Baiolojia na Hisabati ambapo kwa mwaka 2025 tuzo zimetolewa kwa masomo hayo yote.
Nao Judith Haule na Joselini Johanes ni wanafunzi ambao wamepata tuzo hizo, wameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwatambua na kuwaongezea hamasa ya kufanya vizuri zaidi na hatimaye kulitumikia Taifa baada ya kuhitimu Taaluma mbalimbali
“Tunaishukuru sana Mamlaka kwa sababu wamefanya kazi kubwa kuanzia wazo lao mpaka kututafuta nchi nzima kiukweli Mamlaka hii imetutia moyo sana na tunajihisi kuwa na deni kwa Taifa letu” walisema wanafunzi hao.