GCLA YAPONGEZWA KWA KUTOA HUDUMA BORA

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillius Wambura, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kufanya kazi nzuri kupitia uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara wa makosa ya jinai unaofanywa na Mamlaka Hiyo.
IGP Wambura ameyasema hayo Leo Julai 6, 2025 wakati alipotembelea Banda la Mamlaka katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
“Maabara yenu inatusaidia sana niwapongeze, Unajua sasa Hivi kila uhalifu ili kuutolea hukumu unahitaji uchunguzi wa kisayansi, sasa hivi mambo ya ajabu ajabu hayapo tena kwa sababu kuna sayansi ambazo zinaangukia kwenye Maabara zenu, hivyo Maabara yenu inatusaidia sana katika mambo haya”. Alisema IGP Wambura.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inashiriki Maonesho ya Sabasaba kwa kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu majukumu yanayofanywa na Mamlaka hiyo kwa umma.
Maonesho ya 49 ya Sabasaba kwa mwaka 2025 yanafanyika katika viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam yenye kauli mbiu ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba Fahari ya Tanzania yalianza rasmi Juni 28, 2025 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2025.