Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Imewekwa: 29 Nov, 2024
GCLA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema inaendelea kutekeleza matakwa ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya Mwaka 2003 ambayo inawataka kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wadau wanaojishughulisha na kemikali pamoja na jamii kwa ujumla kuhusu matumizi sahihi na salama ya kemikali.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Mussa Kuzumila katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wadau wanaojishughulisha na kemikali kuhusu usimamizi salama wa kemikali yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma Novemba 28, 2024.

“Ndugu washiriki Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeandaa mafunzo haya kwa wadau wanaojihusisha na biashara na matumizi ya kemikali kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo na kufahamu matumizi salama ya kemikali, mafunzo ambayo yanakwenda sambamba na malengo ya maendeleo endelevu kwa watu wote ifikapo mwaka 2030” alisema Kuzumila.

Akizungumzia lengo la mafunzo hayo, Meneja wa Kanda ya Kati, Gerard Meliyo, amesema Mamlaka inakusudia kuhakikisha matumizi ya kemikali yanakuwa salama wakati wote ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa afya za binadamu na mazingira.

“Lengo la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya mafunzo haya kwa wadau hawa ni kuhakikisha kwamba matumizi ya kemikali yanakuwa salama wakati wote ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza katika afya za binadamu na mazingira” alisema Meliyo.

Nae Mshiriki kutoka Kampuni ya LEVOS, Levocatus Makologoto, ameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo na kusema yatakwenda kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku lakini pia yatawasaidia kujua namna ya kujikinga na madhara yatakayotokana na kemikali.