Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI YAWAFIKIA WADAU WA ELIMU

Imewekwa: 14 Sep, 2026
ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI YAWAFIKIA WADAU WA ELIMU

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki imeendesha mafunzo ya Usimamizi na Matumizi Salama ya Kemikali kwa Maafisa Elimu, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu wa masomo ya Sayansi na Wateknolojia wa Maabara, kwa lengo la kutoa elimu ya namna bora ya Uhifadhi na Usimamizi salama wa kemikali katika mazingira ya shule.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Septemba 10, 2026 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Kaimu Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Ibrahimu Kinganije, amewataka na kuwasisitiza wadau hao kuzingatia zaidi taratibu zote za usimamizi na uhifadhi salama wa kemikali katika mazingira ya shule ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

“Niwaombe na kuwasihi kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa za uhifadhi na matumizi salama ya kemikali mashuleni, kwani kwa kufuata taratibu hizi tutaweza kuondokana na ajali zote zinazoweza kusababishwa na uhifadhi usio salama wa kemikali katika mazingira ya shule. Lakini pia kwa zile kemikali taka, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imeandaa namna bora ya uteketezaji wa kemikali hizo” alisema Kinganije.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yameweza kuwakutanisha na wataalamu mbalimbali na kujengeana uwezo wa njia au namna bora ya uagizaji, uhifadhi na matumizi salama ya kemikali mashuleni, lakini pia namna bora ya uteketezaji wa kemikali taka katika mazingira ya shule.