Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

DC DODOMA AIPONGEZA GCLA KUWAFIKIA WAJASILIAMALI WADOGO

Imewekwa: 22 Oct, 2025
DC DODOMA AIPONGEZA GCLA KUWAFIKIA WAJASILIAMALI WADOGO

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), kutoa mafunzo ya usimamizi salama wa kemikali kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha mvinyo katika mikoa ya Kanda ya Kati huku akiwasihi washiriki kuyapa uzito mafunzo hayo ili kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Shekimweri ameyasema hayo Oktoba 16, 2025 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya matumizi salama wa Kemikali kwa wajasiriamali wadogo yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Mafumiko jijini Dodoma.

 “Niwapongeze kwa kuja kushiriki katika mafunzo haya na wengi hapa mnatoka Sekta Binafsi, huwa sio rahisi sana kuwaachia mtoke mjichanganye kama hivi, inamaana moja tu ya kwamba Viongozi wenu wanauelewa wanaona umuhimu wa mafunzo haya” alisema Shekimweri.

Kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa Dodoma, Crispin Kapinga, alisema mafunzo hayo yanalenga kutengeneza uelewa wa matumizi sahihi na salama ya kemikali kwa wajasiriamali wadogo wenye viwanda vya mvinyo.

“kuna malalamiko mengi ya wateja ukipita hata vijiweni utakuta watu wanakwambia wine za Dodoma zina kemikali, baadhi ya wajasiriamali wamekuwa hawazingatii matumizi salama ya Kemikali kama ya ethanol, hivyo imekuwa jambo jema tuwape mafunzo ili kulinda afya ya jamii na mazingira huku uzalishaji ukiongezeka” alisema Kapinga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, amewataka wajasiriamali wadogo wanaozalisha mvinyo kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi na salama ya Kemikali ili kuzalisha bidhaa zenye ubora zisizohatarisha afya ya watumiaji

“Ubora wa bidhaa tunazozalisha ni jambo la msingi sana ni lazima tuzingatie matumizi sahihi na salama ya Kemikali ili kulinda afya za watu na mazingira huku shughuli hii ikiendelea kutuletea maendeleo ya kiuchumi” alisema Ndiyo.

Huku Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga, akisema mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali kutumia Kemikali kwa usahihi na hatimaye kuongeza uzalishaji na kuongeza kipato bila kusababisha madhara.

Washiriki wa mafunzo hayo Dotto Mtenga na Asnath Brembo wamesema kwamba wamejifunza kuwa na matumizi sahihi ya kemikali huku wakiiomba Mamlaka iendelee kutoa Elimu kwa watumiaji wa Kemikali nchini.