BIDII, WELEDI NA UADILIFU: MSINGI WA MAENDELEO KWA WAFANYAKAZI DUNIANI
Wafanyakazi Mkoani Dar es Salaam wametakiwa kuwa washirika wa kweli katika Taasisi, Shirika, wizara au Kampuni wanayofanyia kazi hatua ambayo italeta mafanikio na maendeleao ya Taasisi hizo kusonga mbele.
Kauili hiyo imetolewa Mei 1, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Dar re Salaam Mh.Albert Chalamila wakati akifungua maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kimkoa yalifanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
“Naomba nitoe ufafanuzi kidogo kwenu wafanyakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam maana halisi ya kuwa mfanyakazi ni kuwa mwana hisa katika Taasisi au kampuni unayofanyia kazi, kuwa mwana hisa wa maarifa, mwana hisa wa nguvu au nguvu kazi, kwa maana ya kujitoa kwa dhati katika kampuni unayofanyia kazi kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa nguvu zote kwa maana kuwa kufanya hivyo itaisaidia sana Serikali yetu kuendelea kuleta maendeleo katika nchi yetu.” alisema Chalamila.
Kwa upande wake Meneja wa Rasilimali watu wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Nancy Nombo, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa uadilifu kwa maslahi mapana ya Mamlaka bila kujali changamoto wanazokabiliana nazo kila siku.
“Siku hii ni muhimu kwetu kwa sababu tunatiwa moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kwa weledi na kwa uadilifu. Kama tunavyofahamu hakuna utu bila kazi, hakuna heshima bila kazi, lakini kazi zina changamoto za hapa na pale kitaaluma, na hata katika mahusiano na wenzetu. Kwa hiyo kitu cha msingi ni kuendelea kumuomba Mungu ili aweze kutufanyia wepesi na kutuwezesha kukabiliana na hizo changamoto kwa sababu hakuna namna tunaweza tukaacha kufanya kazi” alisema Nancy.
Maadhimisho ya Mei Mosi hufanyika kila mwaka duniani kote kama jukwaa la kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuhimiza mazingira bora na salama ya kazi.